{"id":"2050","news_title":"Pedro Ajiamini Kabla ya Mbeya City, Dube Aongeza Nguvu Yanga","news_body":"Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Alhamisi, Aprili 16 katika Uwanja wa KMC Complex.\n\nPedro ameweka wazi kuwa licha ya kutambua ugumu wa mchezo huo, ana imani kubwa na wachezaji wake na anaamini watapambana kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu.\n\nAmeeleza kuwa katika mchezo uliopita alifanya mabadiliko ya makusudi ili kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji kurejesha utimamu wa mwili pamoja na kupumzisha nyota wake, jambo analoamini litatoa matokeo chanya katika mchezo ujao.\n\n\u201cNatarajia kuona ufanisi mkubwa zaidi kutoka kwa wachezaji wangu. Malengo yetu ni kupata alama tatu lakini pia kutoa burudani kwa mashabiki wetu,\u201d amesema Pedro.\n\nKocha huyo pia alikumbushia ugumu waliokutana nao kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Mbeya City, akieleza kuwa safari hii watakuwa kwenye mazingira wanayoyazoea, jambo linalowaweka kwenye nafasi nzuri zaidi.\n\n\u201cSisi tupo imara na tunahitaji sana alama tatu. Tunajua hata wao wanazihitaji, lakini kwetu ni muhimu zaidi. Naamini kikosi changu kiko vizuri kimbinu na kiufundi,\u201d aliongeza.\n\nHata hivyo, Pedro amesisitiza umuhimu wa tahadhari, akitaja kuwa Mbeya City ni timu yenye uzoefu na inaweza kuwa hatari endapo watapewa nafasi.\n\nHabari njema kwa Yanga ni kurejea kwa mshambuliaji Prince Dube aliyekuwa nje kutokana na majeraha. Pedro anaamini kurejea kwake kutaongeza makali katika safu ya ushambuliaji, hasa katika kipindi ambacho Laurindo \u2018Depu\u2019 bado hajarejea uwanjani.\n\nAidha, Yanga itamkosa Mwanengo kutokana na majeraha, lakini benchi la ufundi linaendelea kutafuta mbinu mbadala kuhakikisha pengo hilo halionekani.\n\nKwa ujumla, Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali ya juu, ikilenga kuendeleza matokeo mazuri na kuimarisha nafasi yao kwenye mbio za ubingwa.","news_image":"..\/..\/uploads\/smimbazi69dfb025a551a7.79421420image_cropper_D7697A7F-B533-4DD9-AEDE-F3A60B169C81-6522-0000030EDC543426.jpg","gazeti":"habari","posted_time":"2026-04-15 18:34:47.902928","posted_date":"2026-04-15","comments":"0","reads":"144","tmgender":"senior"}